Tafuta

Dominika ya I ya majilio tarehe 1 Desemba 2024 Dominika ya I ya majilio tarehe 1 Desemba 2024 

Dominika ya Majilio:Tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu!

Kristo bado anakuja kwetu,sijui tunamtambua? Je,tunatambua uwepo wake katika kila dakika ya maisha yetu na kuusikiliza ujumbe wake?Huenda tumeshindwa kumuona na hatujawa na utulivu ili kusikia anataka kutuambia nini sababu tunaogopa ujumbe wake utatushtaki na kutuvurugia mambo yetu,hivyo “tunapotezea.”

Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.

U hali gani mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari la Neno la Mungu kutoka hapa Radio vatican, ni wazi kabisa safari ya kutafakari mafumbo ya Kanisa kama alivyotupangia Mama Kanisa Mtakatifu juu ya mwenendo wa liturujia na maadhimisho mbalimbali, hatuna budi kushukuru Mungu sote pamoja na kuendelea kuliadhimisha jina lake milele hata milele, hasa tukikumbuka  kwa Neema na nafasi tuliopewa ya kuadhimisha matakatifu katika Mwaka B wa liturujia ambao umemalizika mwishoni mwa Juma hili, na papo hapo tunapewa zawadi nyingine ya kuendelea kujiunda katika kuutafuta utakatifu tunapofungua pazia  na kuanza , mwaka mpya wa liturujia ndio Mwaka C 2024-2025, Kipindi hiki daima kinafunguliwa na msingi sana katika safari ya ukombozi ambapo ni kipindi cha “Majilio ya mwokozi” kama tujuavyo, Mama mjamzito anapongoja kwa hamu kumpakata na kumnyonyesha mtoto wake mwenyewe huwa katika “majilio”, mkulima anaposubiri kwa hamu mavuno yake huwa katika “majilio”, mwanafunzi anaposubiri matokeo ya mitihani huwa katika “majilio”, wachumba wanaposubiri bila kulala siku yao ya ndoa huwa katika “majilio”, nawe mpendwa wangu katika Bwana katika hilo unalolitarajia upo katika “majilio”

UFAFANUZI

Majilio ni “ujio” ambapo Kristo alikuja katika historia miaka zaidi ya 2024 iliyopita, ujio wa Mtoto wa Bethlehemu, Mwokozi. Bwana wa mabwana na Mungu wa miungu anazaliwa katika unyonge, udhaifu na umasikini katika upweke, giza na ukimya wa usiku akiwahitaji wazazi wa kumuangalia na kumtunza... anasafiri safari ndefu kutoka mbingu za juu kutujia huku bondeni na tangu hapo amedumu kati yetu... Halafu tunayatarajia ‘majilio’ ya pili mwishoni mwa nyakati ambapo Injili ya leo (Lk 21:25-28, 34-36) inaeleza dalili na ishara zake... Bwana wa utukufu atakuja tena, sio kinyonge na kimasikini, hatazaliwa kwenye zizi la wanyama, hatavishwa vinguo vya kitoto na kulazwa horini, hatateswa na kufa bali atakuja kama Mfalme na Hakimu akimlipa kila mmoja wetu ujira katika haki yote.

‘Majilio’ ya tatu ni Kristo anapotujia kila dakika ya uhai wetu katika neno lake, sakramenti zake, ibada na sala za waamini, katika wenzetu na katika huduma za Mama Kanisa na za jamii. Kristo Mfufuka yupo nasi katika safari yetu ya maisha kwa vizazi vyote, kuna nyakati anatushika mkono, kuna nyakati anatubeba mikononi mwake akitulinda, kutuelekeza na kutuongoza vema... na hii ndio furaha ya majilio, kutambua uwepo mtakatifu wa Mwana pekee wa Baba ndani ya nafsi zetu... Kristo anatujia kupitia matukio yetu ya maisha, mazuri au mabaya, ya furaha au huzuni.. anakuja katika yote yanayotupata katika Kanisa na ulimwengu, yupo katika watu wanaotuletea mawazo mapya, wanaoeneza habari njema (euangelion), wanaotamka maneno ya upendo, amani na upatanisho, anakuja katika wale wanaopigania usawa na kujaribu kadiri wawezavyo kuijenga jamii mpya.

Kristo bado anakuja kwetu, sijui tunamtambua? Je, tunatambua uwepo wake katika kila dakika ya maisha yetu na kuusikiliza ujumbe wake? Huenda tumeshindwa kumuona na hatujawa na utulivu ili kusikia anataka kutuambia nini sababu tunaogopa ujumbe wake utatushtaki na kutuvurugia mambo yetu, hivyo “tunapotezea”. Majilio ni majira ambamo tunagundua tumaini jema katikati ya mashaka, uharibifu na kukata tamaa. Ni msimu wa tafakari inayotupa jawabu la swali “hivi ni nini hasa ninaloptakiwa kufanya?”. Ni majira ya kujitahidi kwa nia ya dhati kabisa kuacha dhambi, kushinda tamaa, majaribu na vishawishi, ushindi dhidi ya ulafi, tamaa za mwili, hamu zisizofaa, hasira, ukatili, masengenyo, ulevi, kukosa uaminifu na yanayofanana na hayo.

Majilio ni majira yanayotuandaa na kutujengea uwezo wa kuzishika na kuziishi fadhila za kikristo. Hapo tutafaulu kulishika fundisho hili la Mt. Paulo la kuenenda katika Bwana Yesu na agizo la Kristo katika Injili la kukesha. Kukesha huko ni wito wa kukuza na kuimarisha maisha ya sala na ibada sababu sala hutakasa roho zetu na kuondoa hofu yoyote na kutuandaa kwa tumaini la furaha.  Kristo alizaliwa na kukua kwa lengo maalumu ndio kutufundisha namna ya kupenda, namna ya kuishi, namna ya kujali, namna ya kuwa wanadamu na sio ni lini utakuwa mwisho wa dunia... Mt. Paulo katika somo II (1Thes 3:12-4:2) anatupa dira ya kipindi hiki kitakatifu anaposema “iliyobaki ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu...” hivi tusonge mbele tukilitarajia tumaini lenye heri ambapo yote yatabadilika na hatimaye ushindi mkubwa katika Bwana.

Nabii Yeremia katika somo I (Yer 33:14-16) anahubiri tumaini la kutoka utumwani Babeli walikopelekwa sababu ya dhambi zao wenyewe. Gerusaleme na Hekalu vipo hali ya magofu na ukiwa, ukarabati wake ni mgumu na wa polepole, wanakata tamaa, wanajiuliza ‘Je, Bwana ametuacha kabisa? Je, haendi tena na majeshi yetu? Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, amesahau ahadi na agano lake na wazee wetu?’ wakanung’unika hata kusema ‘Kinachonichoma zaidi ni kwamba Mungu hana nguvu tena…’ Ndipo nabii anawapa moyo na kuwaambia Gerusaleme utakuwa salama na utaitwa jina hili “Bwana ni haki yetu”, wanapata moyo na maisha yanaanza upya.

Hali hii hutukumba pia maishani mwetu, kuharibikiwa na kuvurugikiwa, mara kwa mara tunajikuta utumwani mwa Babeli tunalia, katika hali hiyo tunahitaji majilio ya Kristo ili kurekebisha na kutupa amani. Tujiweke vizuri kusudi kipindi cha majilio kiwe na baraka na kizae matunda ya kudumu katika mioyo yetu ili siku ikifika Kristo azaliwe kwetu, sio kama ratiba, bali kwa uzima wa milele…

Tafakari la Neno la Mungu
30 November 2024, 17:24