Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Allegro
Ratiba Podcast

Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Fadhila ya Kiasi

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Aprili 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, Kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Ni fadhila inayopatikana pia katika nyanja za falsafa za akina Aristotle inayofundisha sanaa ya maisha, ili hatimaye, watu waweze kupata furaha ya kweli katika maisha. Watu waishi kwa kiasi, haki na utauwa ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.  “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Fadhila ya Kiasi
Fadhila ya Kiasi

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia pia fadhila ya subira katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

Kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha.
Kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha.

Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Baba Mtakatifu kuhusu fadhila ya haki, amekazia kuhusu fadhila mbadala zinazowawezesha watu kuishi kwa amani, mtu wa haki daima yuko tayari kuomba msamaha, ni shuhuda wa kanuni maadili na utu wema, kwa hakika watu wa haki ni wachache sana ndani ya jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa haki. Katika maisha ya jamii, kila mtu anapaswa kutendewa kwa haki sanjari na kuheshimu utu wake wake. Fadhila ya haki inadai fadhila nyingine kama: ukarimu, heshima, shukrani, urafiki, uaminifu na kwamba hizi fadhila zinazochangia kuishi pamoja kwa watu vizuri. Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu na uthabiti katika kufuata mema. Yaimarisha uamuzi wa kushindana na vishawishi, kushinda vikwazo vya maisha adili. Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu, hata hofu ya kifo; na kukabiliana na majaribu, na madhulumu. Yamwandaa mtu kuwa tayari hata kujikatalia na kutoa sadaka ya uzima wake kwa ajili ya kutetea haki. Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu. Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu. Rej. KKK 1808.

Papa amewapongeza Mapadre wanaoadhimisha Jubilei zao
Papa amewapongeza Mapadre wanaoadhimisha Jubilei zao

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Aprili 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Ni fadhila inayopatikana pia katika nyanja za falsafa za akina Aristotle inayofundisha sanaa ya maisha, ili hatimaye, watu waweze kupata furaha ya kweli katika maisha. Fadhila ya kiasi “enktateia” inabeba uzito wa juu katika fadhila mbalimbali. Yahifadhi nguvu ya utashi wa kutawala silika na huziweka tamaa katika mipaka ya kile kilicho kinyofu. Mtu wa kiasi huongoza vionjo vya silika kuelekea kilicho chema, na hushikilia busara safi: “Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako.” Kiasi husifiwa mara nyingi katika Agano la Kale. Usizifuate tamaa za roho yako, bali ujizuili uchu wake.” Katika Agano Jipya huitwa: “Kiasi” au “utulivu.” Tunapaswa kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa katika ulimwengu huu. Kuishi vyema si kitu kingine zaidi ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na roho yote na kwa nguvu zote. Toka hapo yatokea kwamba upendo unashikwa wote bila uharibifu (kwa njia ya kiasi.) Hakuna bahati mbaya inayoweza kuusumbua (na hii ndiyo nguvu.) Humtii Mungu peke yake (na hii ni haki), na una makini katika kupambanua vitu, ili usije ukashangazwa na uwongo au udanganyifu (na hii ni busara.) Rej. KKK 1809. Kiasi ni fadhila inayoratibu kile anachofikiri mtu na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa. Hata divai, mtu anapaswa kuitumia kwa kiasi. Mtu wa kiasi huchagua na kupanga maneno yake na kamwe hapendi hasira ivuruge mahusiano na urafiki, kwani kurejesha tena hali hii yataka moyo! Kiasi ni fadhila muhimu sana katika maisha ya kifamilia ili kuratibu kinzani, migogoro na hasira.

Fadhila ya Kiasi inafundisha pia sanaa ya maisha
Fadhila ya Kiasi inafundisha pia sanaa ya maisha

Kila jambo anasema Baba Mtakatifu lina wakati; kuna wakati wa kuzungumza na wakati wa kukaa kimya. Kuna wakati wa kukaa pweke na wakati wa kushirikiana na wengine. Mtu wa kiasi daima anaonesha furaha, amani na utulivu wa ndani. Kuna wakati mtu anapaswa kuzungumza, lakini afanye yote kwa kiasi. Wakati mwingine karipio linasaidia kuliko ukimya unaosimikwa katika hasira na chuki. Mtu mwenye kiasi anajua kuwa hakuna kinachomsumbua zaidi kuliko kuwarekebisha wengine, kwani kwake hili ni jambo muhimu sana, vinginevyo uovu unaweza kutawala. Mtu wenye kiasi anathibitisha matumizi ya kanuni kamili, anadai maadili yasiyoweza kujadiliwa, lakini pia ni mtu mwenye huruma kwa jirani zake. Kwa hiyo zawadi ya mtu mwenye kiasi ni usawa, sifa yenye thamani kama ilivyo nadra. Kwa kweli, kila kitu katika ulimwengu wetu kinatusukuma kuelekea ziada. Badala yake, kiasi huenda vizuri na mitazamo ya Kiinjili kama vile: Udogo, busara, kujificha na  upole. Wale walio na kiasi wanathamini heshima ya wengine, lakini hawaifanyi kuwa kigezo pekee cha kila tendo na kila neno. Mtu mwenye kiasi anafahamu mambo nyeti, anajua kulia na wala haoini aibu. Akichechemea na kuanguka, anainuka na kusimama tena; ni mshindi katika maisha yake ya kawaida; maisha ambayo kwa kiasi fulani yamefichika, lakini pia anatambua kwamba, anawahitaji wengine, ili kukamilisha furaha yake. Kiasi kinamfanya mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha, na kuweza kushirikiana na wengine katika: upole wa urafiki, imani kwa watu wenye hekima, na kuweza kushangaa kwa uzuri wa kazi ya uumbaji. Furaha pamoja na kiasi ni furaha inayositawi katika mioyo ya wale wanaotambua na kuthamini kile ambacho ni muhimu zaidi maishani. Tuombe kwa Mola atupe karama hii: karama ya ukomavu, ukomavu wa umri, ukomavu wa kihisia, ukomavu wa kijamii na zawadi ya kiasi.

Fadhila ya Kiasi
17 April 2024, 15:57

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >
Prev
January 2025
SuMoTuWeThFrSa
   1234
567891011
12131415161718
19202122232425
262728293031 
Next
February 2025
SuMoTuWeThFrSa
      1
2345678
9101112131415
16171819202122
232425262728