Tafuta

Askofu mkuu Agathanghelos akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Chuo cha Kitaalimungu cha Athens nchini Ugiriki, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Askofu mkuu Agathanghelos akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Chuo cha Kitaalimungu cha Athens nchini Ugiriki, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kitengo cha Huduma ya Kitume Cha Kanisa la Kiorthodox: Ujenzi wa Umoja na Ushirika

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amepongeza ushirikiano kati yao na Kanisa Katoliki; mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujikita katika matumaini yanayofumbatwa katika imani, ili kujenga umoja katika tofauti msingi, ili kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo Yesu katika ulimwengu uliogawanyika na kugubikwa na vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ya kijamii. Amemppngeza kwa juhudi zake katika kudumisha: tamaduni, taalimungu na majiundo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kitengo cha Huduma ya Kitume “Apostoliki Diakonia” cha Kanisa la Kiorthodox la Ugiriki, kilianzishwa kunako mwaka 1967 baada ya Sinodi Takatifu kuridhia. Hiki ni chombo rasmi cha Kanisa la Kiorthodox la Ugiriki,  na lengo lake ni kuratibu juhudi zote zinazolenga kuimarisha utume wa uenezaji wa imani na kwa sasa kiko chini ya Askofu mkuu Agathanghelos. Akiwa ameambatana na ujumbe kutoka Chuo cha Kitaalimungu cha Athens nchini Ugiriki, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amepongeza ushirikiano kati yao na Kanisa Katoliki; mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujikita katika matumaini yanayofumbatwa katika imani, ili kujenga umoja katika tofauti msingi, ili kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo Yesu katika ulimwengu uliogawanyika na kugubikwa na vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ya kijamii.

Majadiliano ya kiekumene yanasimikwa katika umoja na ushirika
Majadiliano ya kiekumene yanasimikwa katika umoja na ushirika

Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Agathanghelos pamoja na ujumbe wake, ambaye tangu kuteuliwa kwake, amekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha umoja na udugu miongoni mwa Wakristo kama alivyo Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima, Mtu wa imani thabiti, na mchungaji mwema, ambaye kwa nyakati tofauti tofauti amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na hasa wakati wa hija yake ya kitume nchini Ugiriki. Amewashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuuonesha kwa Tume ya Kanisa Katoliki ya Ushirikiano wa Utamaduni. Katika miaka ya hivi karibuni ambapo watu wa Mungu nchini Ugiriki wameshuhudia athari za mtikisiko wa uchumi: Kitaifa na Kimataifa sanjari na athari za maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Kitengo cha Huduma ya Kitume: Lengo ni kueneza imani
Kitengo cha Huduma ya Kitume: Lengo ni kueneza imani

Kwa umoja wao, waliweza kushirikiana katika kukuza na kudumisha miradi ya pamoja katika masuala ya elimu na utamaduni. Baba Mtakatifu amempongeza Askofu mkuu Agathanghelos kwa kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika kukuza na kudumisha tamaduni, taalimungu na majiundo ya kiekumene kwa vijana wa kizazi kipya. Ni katika muktadha huu, vijana hawa wakiwa wameimarishwa katika matumaini yanayosimikwa katika imani wanaweza kuvunjilia mbali uadui kati ya Makanisa, hali ya kutoelewana na maamuzi mbele ambayo yameendelea kuwepo kwa miaka mingi kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Umefika wakati wa kutambuana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu, tayari kutolea ushuhuda wa upendo angavu wa Kristo Yesu, na hasa katika ulimwengu uliogawanyika na kugubikwa na vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ya kijamii.

Muhimu majiundo ya kiekumene kwa vijana wa kizazi kipya
Muhimu majiundo ya kiekumene kwa vijana wa kizazi kipya

Chuo cha Kitaalimungu cha Athens nchini Ugiriki, mwaka huu, kitatoa makazi kwa wanafunzi wa Kanisa Katoliki wanaojifunza Lugha ya Kigiriki na Kanisa la Kigiriki katika ujumla wake. Baba Mtakatifu tangu sasa anapenda kuwashukuru kwa moyo huu wa umoja na ushirikiano. Kwa Wakristo kutembea kwa pamoja, kwa kusali katika umoja na mshikamano, ni sehemu ya maandalizi ya kupokea zawadi ya umoja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kama matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu, ili kujenga na kuimarisha umoja na ushirika kati ya Wakristo, hata katika tofauti zao msingi. Hadi sasa anasema Baba Mtakatifu Francisko jambo la msingi kwa Wakristo ni kutembea kwa pamoja, kusali na kufanya kazi kwa umoja, lakini tarehe ya umoja wa Wakristo, hilo linabaki kuwa ni fumbo la imani. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amewaombea neema na baraka nyingi katika maisha na utume wao.

Uekumene
16 May 2024, 14:45