Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Mei 2024 amewatakia waamini wote, wingi wa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Mei 2024 amewatakia waamini wote, wingi wa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu.   (Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste: Mwanzo wa Kanisa na Siku ya Walei Duniani

Baba Mtakatifu Francisko amewatakia waamini wote, wingi wa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kristo Yesu, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi ndani ya Kanisa “Magisterium”; katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu, Katika sala ambako anawaombea; katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika Ishara na maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya ukombozi. Rej. KKK 683-730 Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. KKK 731-747.

Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa
Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Mei 2024 amewatakia waamini wote, wingi wa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kristo Yesu, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, wabatizwa wanakamilishwa na hivyo kufanana na Kristo Yesu na kwamba, Yeye mwenyewe akamilishe yale yote aliyoanzisha ndani mwao, kwa kuendelea kujinyenyekeza chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, aweze kuwasha ndani ya nyoyo za waamini moto wa upendo. Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu, Ubatizo na kuzaliwa kwa Kanisa na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila Taifa chini ya mbingu, Rej. Mdo 2: 1-11. Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa kuwa ni: moja, takatifu, katoliki na la mitume kuzaliwa. Hii ni siku ya waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu. Huu ni mwaliko wa kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe. Kugundua ile zawadi ya kuinjilishwa na kwa kupokea zawadi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, “Kerygma”, na hatimaye kufanyika kuwa ni sehemu ya Mama Kanisa anayezungumza lugha zote na ndiyo maana ya kuwa ni Katoliki.

Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Baba Mtakatifu anasema, kabla ya mtu kuwa ni: Mtume, Padre, Askofu au Kardinali walikuwa ni Waparthi, Wamedi na Waelami, kielelezo makini cha neema ya Injili kwa watu wa Mataifa. Ni katika asili ya watu wa Mungu, Roho Mtakatifu ametenda kazi ya kutangaza na kushuhudia Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu, Fumbo ambalo limewafikia watu wa Mataifa katika lugha zao za asili, kupitia kwa wazazi, makatekista, mapadre, wamisionari bila kuwasahau mabibi na mababu. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu Francisko wa kuwa ni wainjilishaji, kwa sababu kwanza kabisa wameinjilishwa, tayari kupyaisha kumbukumbu na zawadi ya imani. Pentekoste kama Ubatizo ni tukio ambalo Mwenyezi Mungu anaendelea kulipyaisha Kanisa na watoto wake kila wakati, ili kuendelea kuishi leo ya Mungu mintarafu imani inayosimikwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni wito wa kusikilizana, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi na uaminifu katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa. Waamini wajifunze kuwa wamoja katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, daima watambue kwamba, wanaye Roho Mtakatifu, Mwalimu kiongozi, anayewawezesha kutembea huku wakiwa wameshikamana. Roho Mtakatifu anaunda tofauti na kukuza umoja, ndiye kiongozi mpole na mwenye nguvu, ambaye watu wote wateule na watakatifu wa Mungu wanajiaminisha kwake, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Sherehe ya Pentekoste
15 May 2024, 15:27