Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni Sanjari na Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2024. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni Sanjari na Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2024.  (AFP or licensors)

Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Teknolojia ya Akili Mnemba

Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yananogeshwa na kauli mbiu “Akili Mnemba (AI) na Hekima ya Moyo: Kuelekea katika Mawasiliano Imara ya Mwanadamu.” Ni kwa kupata hekima ya moyo pekee, ndipo mwanadamu anaweza kufasiri masuala ya wakati huu na hatimaye kugundua tena njia ya mawasiliano kamili ya mwanadamu. Papa amewashukuru na kuwapongeza wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano kwa kazi na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni Sanjari na Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, Dominika tarehe 12 Mei 2024 amesema kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Akili Mnemba (AI) na Hekima ya Moyo: Kuelekea katika Mawasiliano Imara ya Mwanadamu.” Ni kwa kupata hekima ya moyo pekee, ndipo mwanadamu anaweza kufasiri masuala ya wakati huu na hatimaye kugundua tena njia ya mawasiliano kamili ya mwanadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano kwa kazi na utume wao! Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafunagamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za watu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba iwe inategemewa. Kuwepo na chombo kitakachodhibiti masuala ya maadili, haki msingi za watumiaji na waathirika. Teknolojia ya akili mnemba itumie pia tafiti za kitekolojia na kisayansi, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Teknolojia ya Akili Mnemba
Teknolojia ya Akili Mnemba

Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo na kwamba, itakuwa na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, kwa kuweka msingi wa ufahamu hadi kufikia ukweli na kamwe teknolojia hii isitumike kwa ajili ya kusambaza habari za kughushi na hivyo kusababisha njia za mawasiliano ya jamii kutoaminika, kwa kujikita katika masuala ya ubaguzi; kuingilia katika michakato ya uchaguzi, kwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kukomaza ubinafsi; mambo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa cha kutafuta na kudumisha amani. Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia kwani kuna hatari kushindwa kuchakata takwimu nyingi na hivyo kusababisha ukosefu wa haki na maamuzi mbele katika mazingira zilimotoka takwimu hizi, kumbe, binadamu anapaswa kufanya tathmini na hatimaye, kutoa uamuzi wa mwisho. Hapa, kuna haja ya kufikiria ukomo katika teknolojia kamwe teknolojia isitumike kuzalisha utajiri kwa watu wachache ndani ya jamii na hivyo kuhatarisha demokrasia na amani katika ujumla wake.

Teknolojia ya Akili Mnemba ilete maboresho ya kweli
Teknolojia ya Akili Mnemba ilete maboresho ya kweli

Itakumbukwa kwamba, kila mwaka Baba Mtakatifu anatoa ujumbe katika Maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Mwaka huu ikiwa ni maadhmisho ya 58, Baba Mtakatifu anatoa ujumbe unaobeba kauli mbiu: “Akili Mnemba (AI) na Hekima ya Moyo: Kuelekea katika Mawasiliano Imara ya Mwanadamu.” Kauli mbiu hii ni mwendelezo wa ujumbe ambao Baba Mtakatifu aliutoa katika maadhimisho ya Siku ya Amani Ulimwenguni ambapo alikazia kuhusu maendeleo ya mifumo ya akili mnemba, yanavyoathiri ulimwengu wa mawasiliano. Hivyo, hupelekea katika maswali ya kina kuhusu asili ya mwanadamu, utofauti wetu na hatima ya viumbe “homo sapiens” katika kipindi hiki cha akili mnemba. Baba Mtakatifu anauliza: Je inawezekana kila mmoja wetu leo kubaki kuwa mtu aliyekamilika pamoja na mabadiliko ya tamaduni na kuishi katika lile lengo jema na zuri? Ni katika muktadha huu ambapo Baba Mtakatifu anaona jinsi ilivyo ngumu kuishi wito wetu kama wanadamu akielezea kuwa akili mnemba kama changamoto inayokabili ulimwengu wa leo. Kumbe ni muhimu kutambua kuwa akili ya mwanadamu ina hazina kubwa kuliko ile iliyokuwa nayo mashine, hazina hiyo ni moyo na hisia. Ikumbukwe kuwa hiki ni kipindi ambacho katika historia ya mwanadamu, kuna utajiri wa teknolojia lakini kuna umaskini wa utu. Hivyo Baba Mtakatifu anasema kuwa ni muhimu zaidi kutafakari kwa pamoja, na katika kutafakari huko lazima kuanze na moyo wa mwanadamu. Anaendelea kwa kusema “Mashine zina uwezo mkubwa sana ambao unaweza kuwa zaidi ya uwezo wa mwanandamu, hasa katika kutunza na kuunganisha data na nyaraka mbalimbali, lakini ni vyema kukumbuka kuwa ni mwanadamu pekee ndio mwenye uwezo wa kuleta maana ya hizi data”.

Akili Mnemba na Hekima ya Moyo
Akili Mnemba na Hekima ya Moyo

Baba Mtakatifu amezungumzia sio tu kuhusu swala la fursa ya akili mnemba lakini pia madhara yake. Mifumo ya akili mnemba inaweza kusaidia kushinda ujinga na kukuza katika kubadilishana habari kati ya watu na vizazi vyao. Wakati huo huo, hata hivyo, mifumo hii pia inaweza kuwa chanzo cha "uchafuzi wa utambuzi", yaani, upotovu wa ukweli kwa maelezo ya uongo na ya uzushi, ambayo huchukuliwa kuwa ya kweli na kuenea. Amesisitiza kuhusu kuchukua hatua za kuzuia, kupendekeza mifano ya usimamizi wa maadili, kuzuia matumizi ya mifumo ya akili mnemba katika kuzalisha madhara mabaya, ubaguzi katika jamii, na kupambana na matumizi mabaya ya mifumo hii ili kupunguza utofauti. Kumbe matumizi ya akili mnemba yanaweza kutoa mchango mzuri katika sekta ya mawasiliano, ikiwa haiondoa jukumu la uandishi wa habari na kuthamini taaluma ya mawasiliano, na kumfanya kila mtu wa mawasiliano atambue zaidi majukumu yake, na kuwezesha watu wote kuwa, kama wanavyopaswa, washiriki wenye utambuzi katika kazi ya mawasiliano. Hivyo ni wajibu na jukumu la kusikiliza kabla ya kueleza ukweli. Ni kupitia taaluma hii ya uandishi wa Habari ndipo kuna kudhibiti changamoto ya akili Mnemba kwa kuendelea kusaidia watu kutofautisha kati ya ukweli na habari za uongo. Hakika bado kuna maswali mengi sana ambayo Baba Mtakatifu anatualika kutafakari hasa katika uenezaji habari na mifumo ya akili mnemba. Maswali haya yanahusisha vitu kama vile taaluma na heshima ya wafanyakazi katika nyanja za habari na mawasiliano, ushirikiano wa majukwaa ya habari, uwazi katika uendeshaji wa “algorithm,” uwazi wa uenezwaji wa habari, utambuzi wa vyanzo vya habari, usawa wa habari hata katika nchi zinazoendelea.

Teknolojia ya Akili Mnemba Siku ya 58 ya Mawasiliano Ulimwenguni
Teknolojia ya Akili Mnemba Siku ya 58 ya Mawasiliano Ulimwenguni

Baba Mtakatifu anasema kuwa “majibu ya maswali haya yataamua kama akili mnemba itaishia kuunda tabia mpya kulingana na upatikanaji wa habari na hivyo kusababisha aina mpya za unyonyaji na usawa. Au, itasababisha usawa mkubwa kwa kukuza habari sahihi”. Yote haya yatategemea na sisi wenyewe, na itabaki kuwa ni jukumu letu kama kuamua ikiwa tutakuwa chakula cha mifumo hii ya utumwa au tutalisha mioyo yetu kwa uhuru ambao bila huo hatuwezi kukua katika hekima. Baba Mtakatifu anamalizia kwa kutoa wito kwa kila mmoja wetu “kutafuta hekima iliyopo kabla ya vitu vyote, ili ubinadamu wetu usipoteze uwezo wake (taz. Sir 1:4). Hii itapelekea katika kuweka misingi thabiti na kufanya akili mnemba kuwa katika huduma ya mawasiliano ya kibinadamu.” Kwa maneno mengine, Mwanadamu hapaswi kuwa chakula cha kukimbizwa na habari, mawasiliano yanabaki daima kuwa ya kibinadamu.

Upashanaji Habari 2024

 

13 May 2024, 15:35