Tafuta

Msiogope Dhoruba na Upepo Mkali: Muhimu Imani na Ujasiri Maishani!

Lengo kuu la Kristo Yesu la kuwapatisha katika dhoruba na upepo mkali lilikuwa ni kuwaimarisha katika imani na kuwajengea ujasiri zaidi. Uzoefu na mang’amuzi haya yaliwawezesha Mitume kutambua nguvu na uweza wa Kristo Yesu kati yao, wakaimarika zaidi na hivyo kuondoakana na woga wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hii ni changamoto kwa waamini kujiaminisha kwa Mungu katika sala, wakati wa shida na magumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 12 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mwinjili Marko anamwonesha Kristo Yesu akiwa chomboni pamoja na Mitume wake kwenye Ziwa la Galilaya ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia. Ghafla ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Kristo Yesu alikuwapo kwenye shetri, amelala juu ya mto, wakamwamsha, akaamka, akaukemea upepo, upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Ni Kristo Yesu aliyekuwa amewaambia Mitume wake kuvuka mpaka ng’ambo ya pili. Itakumbukwa kwamba, Mitume walikuwa ni wataalam katika sekta ya uvuvi na kwamba, bahari ilikuwa ni viunga vyao vya kazi na maisha, lakini dhoruba kuu ya upepo na mawimbi yalitishia maisha yao. Pengine Kristo Yesu alitaka kuwapima imani yao! Lakini hakuwaacha pweke, alikuwa pamoja nao chomboni, katika hali ya utulivu, kiasi hata cha kulala usingizi!

Tafakari: Kristo Yesu alitaka kuwapima Mitume wake imani
Tafakari: Kristo Yesu alitaka kuwapima Mitume wake imani

Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Katika maisha na historia yake, Kanisa limekumbana na dhoruba mbalimbali, lakini limeweza kuvuka yote haya na kusonga mbele kwa sababu Kristo Yesu ndiye nahodha wa chombo hiki na kamwe hajawahi kulala na kukiacha chombo kizame! Dhoruba ilipokuwa inapamba moto, uwepo wake, uliwahakikishia usalama, ukawatia moyo na kuwaamshia imani, ili waweze kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika kukabiliana na matatizo na changamoto zitakazo kuja mbeleni. Lengo kuu la Kristo Yesu lilikuwa ni kuwaimarisha katika imani na kuwajengea ujasiri zaidi. Uzoefu na mang’amuzi haya yaliwawezesha Mitume kutambua nguvu na uweza wa Kristo Yesu kati yao, wakaimarika zaidi na hivyo kuondokana na woga wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Anawashirikisha Mwili na Damu yake Azizi
Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Anawashirikisha Mwili na Damu yake Azizi

Baada ya kuvuka na kushinda jaribio hili wakiwa na Kristo Yesu kati yao, wataweza kufaulu kupambana na changamoto za maisha, hadi Msalabani, huku wakiwa tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hata kwa kumwaga damu yao, kama mashuhuda wa imani. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Juni 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hivi ndivyo inavyotokea kwa waamini wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anawaunganisha pamoja naye, anawakirimia Neno lake na kuwalisha kwa Mkate na kuwanywesha kwa Damu yake Azizi, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwashirikisha jirani yale waliyosikia na kuyaona kwa macho yao bila kusahau matatizo na changamoto za maisha. Kristo Yesu yuko pamoja na wafuasi wake, ili kuwasaidia na kuwaokoa, ili hata wafuasi wake, baada ya kujiaminisha na kutumainia nguvu zake waweze kuambatana na Kristo Yesu, kwa kutumainia nguvu zake ambazo zinapita uwezo wao, waendelee kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu na kwamba, kwa uwepo wa Kristo kati pamoja nao wanaweza kusaidia kuukuza na hivyo kushinda vizuizi vyote!

Wakristo wanaitwa na kutumwa Kuinjilisha
Wakristo wanaitwa na kutumwa Kuinjilisha

Baba Mtakatifu Francisko anataka waamini kujiuliza swali hili, katika nyakati za majaribu; Je, wanaweza kukumbuka nyakati hizi katika maisha yao; uwepo na msaada wa Mungu? Dhoruba inapotokea; Je, kama waamini wanajiruhusu kuelemewa na msukosuko huo au anajishikamanisha na Kristo Yesu ili kupata: utulivu na amani ya ndani katika sala, ukimya, Kuabudu Ekaristi Takatifu sanjari na kushiri imani kindugu? Bikira Maria aliyepokea mapenzi ya Mungu kwa unyenyekevu na ujasiri, awaombee nguvu, utulivu sanjari na kujizamisha ndani mwake.

Imani na Ujasiri
23 June 2024, 14:31

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >