Tafuta

Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho mintarafu historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho mintarafu historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. 

Injili na Pango la Noeli Ni Msaada wa Tafakari ya Fumbo la Umwilisho!

Injili na Pango la Noeli ni msaada katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili hatimaye, kufuata ile Njia ya Msalaba kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Bethlehemu pamoja na picha alizowahi kuona kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Alilitengeneza Pango la Noeli, Siku 15 kabla ya Sherehe ya Noeli kama kumbukumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho. Ilikuwa ni tarehe 25 Desemba 1223 watawa Wafranciskani kutoka sehemu mbalimbali za dunia walipofika kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio. Pango likapambwa kwa uwepo wa mahujaji na wanyama mbalimbali na Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa Pangoni humo, ili kuonesha uhusiano wa dhati kati ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Huu ndio ukuu na utakatifu wa Fumbo la Umwilisho, mwaliko kwa waamini kuamsha tena mshangao kwa unyenyekevu wa Mungu aliyefanyika Mtoto!

Maana na umuhimu wa Pango la Noeli katika maisha na utume wa Kanisa
Maana na umuhimu wa Pango la Noeli katika maisha na utume wa Kanisa

Mara ya kwanza, Pango la Noeli halikuwa na sanamu mbalimbali kama zinavyonekana wakati huu. Pole pole, Pango la Noeli likapambwa kwa Sanamu ya Mtoto Yesu aliyelazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Na wote walioshuhudia tukio hili wakarejea makwao wakiwa wamesheheni furaha kubwa nyoyoni mwao. Haya ni matunda ya uinjilishaji uliofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, kiasi kwamba, mafundisho yake, hadi leo hii yanaendelea kugusa sakafu ya maisha ya waamini kwa njia ya imani. Madhabahu ya Greccio yamekuwa ni kimbilio la watu wanaotaka kusali na kutafakari katika hali ya utulivu na kimya kikuu. Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu, ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki wa kijamii unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru!

Ishara ya Kushangaza
Ishara ya Kushangaza

Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili hatimaye, kufuata ile Njia ya Msalaba kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anafafanua kwa kina na mapana kuhusu: Pango la Noeli, Asili yake, Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kuhusu Pango kama ishara ya uinjilishaji pamoja na alama za Pango la Noeli. Pango la Noeli ni mchakato unaojikita katika kueneza na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutafakari na kuhisi na kuonja uwepo wa Mungu kwa binadamu; kuhisi na kuonja uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Baba Mtakatifu anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Kwa Waraka huu wa Kitume, uliochapishwa tarehe 1 Desemba 2019, Papa Francisko anapenda kuwahamasisha waamini kuendeleza Mapokeo ya kuandaa Pango la Noeli kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, magerezani na kwenye maeneo ya wazi, kama kielelezo cha ibada katika Fumbo la Umwilisho.

Pango la Noeli, Asili yake na Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi: Uinjilishaji
Pango la Noeli, Asili yake na Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi: Uinjilishaji

Ni katika muktadha wa maana, umuhimu wa Pango la Noeli, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 22 Desemba 2024 amebariki Sanamu za Mtoto Yesu, zinazowekwa kwenye Pango la Noeli. Baba Mtakatifu aliwaonesha waamini Sanamu ya Mtoto Yesu, aliyozawadiwa na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la “Santa Fè” kutoka nchini Ecuador. Hii ni Sanamu iliyochongwa na watu asilia wa Ecuador. Hiki ni kielelezo cha Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika Mwili na kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Sherehe za Noeli, kiwe ni kipindi cha upendo, ukarimu na mshikamano! Baba Mtakatifu amesema kwamba, Dominika tarehe 22 Desemba 2024 alipata nafasi ya kukaa pamoja na watoto na mama zao wanaohudumiwa kwenye Zahanati ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican, inayosimamiwa na kuongozwa na Shirika la Masista wa Huruma wa Mtakatifu Vinsenti wa Paulo. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko watoto hawa waliokuwa wengi wamemjaza furaha moyoni mwake na kusema kwamba, hakuna mtoto anayezaliwa kwa bahati mbaya! Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na madhara ya vita sehemu mbalimbali za dunia, anamwomba Mwenyezi Mungu ili kweli Sherehe za Noeli iwe ni fursa ya kusitisha vita, kielelezo cha ukatili wa kutisha dhidi ya watoto wadogo!

Pango la Noeli 2024
23 December 2024, 14:21