Tafuta

2024.12.16 Papa amekutana na Ujumbe wa Baraza la Wamethodisti Ulimwenguni. 2024.12.16 Papa amekutana na Ujumbe wa Baraza la Wamethodisti Ulimwenguni.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa na Wamethodist:Kumbu kumbu ya Nikea ni mwaliko wa kuelekea Umoja

Baba Mtakatifu akikutana na ujumbe kutoka Baraza la Methodist Ulimwenguni,katika hotuba alikumbuka kumbukumbu ya miaka 1700 ya Baraza la I la Kiekumene la Nikea:linatukumbusha kwamba tunakiri imani sawa na tuna wajibu sawa wa kutoa ishara za matumaini zinazoshuhudia uwepo wa Mungu duniani."Papa alitoa mwaliko wa kutembea pamoja katika upendo na mazungumzo,kwani Wamethodisti na Wakatoliki walikuwa hawaaminiani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Desemba 2024 akikutana na Uwakilishi wa Baraza la Wamethodisti Ulimwenguni amewakaribisha kwa furaha na kumsalimia Askofu Debra Wallace-Padgett na Mchungaji Reynaldo Ferreira Leão-Neto. Amewatakia heri na baraka wanapoanza majikumu mapya ya utumishi wao kama Rais na Katibu Mkuu wa Baraza la Wamethodisti Ulimwenguni. Kwa kipindi kirefu Wamethodisti na Wakatoliki walikuwa wametengana na kuhofia kila mmoja wao. Leo, hata hivyo, tunaweza kumshukuru Mungu kwamba, kwa karibu miaka sitini, tumekuwa tukiendelea pamoja katika ujuzi wa kubadilishana, kuelewana na upendo. Hii inasaidia kuimarisha ushirika wetu wa pamoja. Papa amesema kuwa “kwa kujifungua sisi kwa sisi  kumetuleta karibu na kutufanya tutambue kuwa upatanisho ni kazi ya moyo. Moyo wa Bwana Yesu unapogusa mioyo yetu, yeye hutubadilisha. Hivi ndivyo jumuiya zetu zitaweza kuunganisha akili na nia zao tofauti ili kujiruhusu kuongozwa na Roho kama kaka na dada.”

Safari ndefu

Papa Francisko alisisitiza kuwa “Hii ni safari ambayo inachukua muda, lakini lazima tuendelee kwenye njia hiyo, daima tukizingatia Moyo wa Kristo, kwa sababu ni kutoka kwa Moyo huo tunajifunza uhusiano mzuri kati yetu na kutumikia ufalme wa Mungu (taz. Dilexit Nos, 28). Mwaka ujao, yaani (2025), Wakristo duniani kote wataadhimisha mwaka wa 1700 wa Baraza la Kwanza la Kiekumene, la Mtaguso wa Nikea. “Tukio hili linatukumbusha kwamba tunakiri imani sawa, na hivyo kuwa na wajibu uleule wa kutoa ishara za matumaini zinazotoa ushuhuda wa uwepo wa Mungu duniani.”

Kutembea pamoja ili kuwa wamoja

Kwa hakika, Papa alisema huu ni “wito kwa Makanisa yote na Jumuiya za Kikanisa ili kudumu katika njia inayoelekea kwenye umoja unaoonekana na kutafuta njia za kuitikia kikamilifu sala ya Yesu ya: ‘ili wote wawe kitu kimoja’.” (Spes Non Confundit, 17).” Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wachungaji na wataalimungu ambao wamehudumu katika Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Mazungumzo kati ya Baraza la Wamethodist Ulimwenguni na Kanisa Katoliki, na vile vile amewahimiza washiriki wa sasa kuendelea na juhudi hizo hizo. Kwa kuhitimisha, ametoa shukrani za dhati kwao na kwamba wabaki katika umoja na maombi na kuwatakia Noeli Njema.

Papa na Methodist
16 December 2024, 17:07