Tafuta

2024.12.16 Wawakilishi wa Jumuiya ya kifilipini nchini Hispania. 2024.12.16 Wawakilishi wa Jumuiya ya kifilipini nchini Hispania.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko:Kanisa ni nyumba yenye joto la kukaribisha wote

Papa Francisko tarehe 16 Desemba alikutana na wawakilishi wa Jumuiya ya Wafilipini wanaoishi nchini Hispania,katika fursa ya miaka 25 baada ya kuanzishwa kwa Parokia yao binafsi huko Barcelona.Papa amebainisha kwamba:“Kanisa ni nyumba yenye joto na ya kukaribisha kwa wahamiaji.Na wafilipini kila eneo wanatoa ushuhuda.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Desemba 2024 alikutana na wawakilishi wa Jumuiya ya Wafilipini ambao wanaishi Hispania katika fursa ya maadhimisho ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Parokia yao Binafsi huko Barcelona nchini Hispania. Papa akianza hotuba yake alionesha furaha yake ya kukutana nao na kwamba walitaka kuita utume wao huko Madrid "Tahanan", na kwamba ni “neno zuri ambalo tunaweza kulitafsiri kama makazi. Na ni kweli, Kanisa, mahali popote tuendapo, daima ni nyumba yetu, nyumba yenye joto na ukarimu, na leo nyumba ya Petro pia ni kama nyumba kwenu. Karibu!”

Papa alisisitiza kuwa alivyoona kwamba huko Madrid wana makao yao makuu katika parokia ya Nuestra Señora del Espino yaani Mama Yetu wa miiba). Na hili ilinifanya awafikirie watu wengi wahamiaji ambao, mbali na kupata nyumba hiyo yenye joto na ukaribishaji, badala yake wanakumbana na matatizo na kutokuelewana mara nyingi, jambo ambalo huwa ni kama miiba dhidi yao. Mama yetu mwenyeheri  anajionesha kwetu juu ya miiba hii, ili tusipoteze tumaini na kuweza kukabiliana na shida, tukiamini ulinzi na msaada wake.

Miaka 25 tangu kuanzisha Parokia ya kifilipino Hispania 

Sababu ya ziara hiyo  ni kumbukumbu ya miaka 25 ya kusimamishwa kisheria kwa parokia ya kibinafsi ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili na ya Mtakatifu  Laurent Ruiz, huko Barcelona. Mtakatifu Laurent ni sura nzuri kwa sababu, kwa upande mmoja, anazungumza nasi kuhusu ushirikiano wa tamaduni. Kwa hakika, familia yake, kama ile ya Kardinali Tagle, ilikuwa na asili ya Kichina na Kifilipino ambayo, pamoja na yule Mhispania aliyempatia imani, waliunda mchanganyiko bora. Kwa upande mwingine, ilimbidi kuachana na ardhi yake kwa sababu ya ukosefu wa haki, katika kesi yake kukashifiwa, kama watu wengi ambao hadi leo wanalazimika kuhama ili kuokoa maisha yao au kutafuta maisha bora ya baadaye.

Ushuhuda na kujitoa maisha

Hatimaye, mara tu alipofika katika nchi ambayo ilipaswa kumkaribisha, Mungu alimwomba ashuhudie imani yake kwa uthibitisho mkubwa zaidi wa upendo yaani wakutoa uhai wake mwenyewe. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amewahimiza waige mifano yao, wote wawili ambao walipaswa kuacha nchi yao, lakini wote wawili walifanya hivyo kwa kumkumbatia Yesu, wote wawili walikumbana na magumu bila kupoteza matumaini na wote wawili ni mifano ya maisha ya kujitolea kumtumikia Mungu katika Ndugu. Kwa kufanya hivyo, Papa ameongeza kusema “tutaweza kujenga "Tahanan" yetu, nyumba hiyo yenye joto na kukaribisha ambako, kama Mama, Kanisa letu lazima liwe hivyo.”

Ushuhuda wa wafilipini ulimwenguni

Mungu Mwana awakubariki na Bikira Mtakatifu awalinde.  Vile vile Papa Francisko ameonesha juu ya kumbu kumbu yake nzuri alipotembelea ardhi yao katika ziara yake na kwamba waliudhuria waamini milioni saba katika Misa huko Manila na kisha Misa nyingine huko Tocloban. Kwa mvua na upepo, anakumbuka walivyolazimika kuondoka haraka kwa sababu ya dhoruba ilikuwa inafika na vinginevyo wasingeweza kuruka angani. Wafilipini ni wanaume na  wanawake wa imani. Baadhi yao  wanafanya kazi jijini Vatican na inapendeza sana, imani waliyonayo na ushuhuda wanaotoa ni wa ajabu. Kwa njia hiyo amewaomba waendelea kutoa ushuhuda katika jamii hii ambayo imekuwa tajiri kupita kiasi, na uwezo mkubwa wa kutosha. Na shukrani kwa kile wanachofanya. Papa amehitimisha kwa Baraka.

Papa kwa Jumuiya ya Wafilipini, Hispania
16 December 2024, 17:23