Katibu Mkuu wa UN anatoa wito wa kuunga mkono watu wa Palestina katika siku ya Mshikamano!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,(UN) Bwana Antonio Gutteres alitoa ujumbe wake katika fursa ya kuelekea Kilele cha “Siku ya Mshikamano na watu wa Palestina” itakayofanyika tarehe 29 Novemba 2024. Katika Ujumbe huo, Bwana Antonio anaandika kuwa “ Kila mwaka katika siku hii, jumuiya ya kimataifa inasimama kidete na mshikamano kwa ajili ya utu, haki, usawa na kujitawala kwa watu wa Palestina. Maadhimisho ya mwaka huu ni ya uchungu sana kwani malengo hayo ya msingi yako mbali sana kama yalivyowahi kuwa. Hakuna kinachohalalisha shambulio la kigaidi la Oktoba 7 lililofanywa na Hamas na kuwateka mateka. Na hakuna kinachohalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina.
Kiongozi huyo Mkuu wa UN anabainisha kuwa “Hata hivyo, zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Gaza ni magofu, zaidi ya Wapalestina 43,000 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto - wameripotiwa kuuawa, na mzozo wa kibinadamu unazidi kuwa mbaya zaidi siku hadi siku. Hii inatisha na haina udhuru.Wakati huo huo, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ikiwa ni pamoja na Yerusalem Mashariki, operesheni za kijeshi za Israel, upanuzi wa makazi, kufukuzwa, ubomoaji, ghasia za walowezi na vitisho vya kunyakuliwa vinasababisha maumivu zaidi na dhuluma.”
Kiongozi huyo aidha anasisitiza kwamba “Wakati umepita wa usitishaji mapigano mara moja na kuachiliwa huru bila masharti kwa mateka wote; kukomesha kukaliwa kwa mabavu eneo la Palestina kinyume cha sheria - kama ilivyothibitishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Baraza Kuu; na maendeleo yasiyoweza kutenduliwa kuelekea suluhisho la Serikali mbili, kulingana na sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa - Israeli na Palestina zikiishi bega kwa bega kwa amani na usalama, na Yerusalem kama mji mkuu wa Mataifa yote mawili.”
Bwana Guterres ametoa wito kwamba “Kama jambo la dharura, ninaomba uungwaji mkono kamili wa misaada ya kibinadamu inayookoa maisha kwa watu wa Palestina - hasa kupitia kazi ya UNRWA, ambayo inawakilisha njia isiyoweza kubadilishwa kwa mamilioni ya Wapalestina. Umoja wa Mataifa utaendelea kusimama katika mshikamano na watu wa Palestina na haki zao zisizoweza kupokonywa za kuishi kwa amani, usalama na utu.”