Nikaragua,mapadre wawili zaidi wakamatwa
Osservatore Romano
Polisi tarehe 28 Desemba 2023 walimkamata Monsinyo Carlos Avilés na Padre Héctor Treminio, ambao wote wawili ni makamu na mweka hazina wa Jimbo katoliki la Managua. Kulingana na vyanzo vya ndani, mapadre hao wawili walikamatwa baada ya kumuombea Askofu Rolando José Álvarez Lagos, wa Jimbo la Matagalpa na msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Estelí, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 26 jela, bila kufuata utaratibu, kwa kisingizo cha makosa ya uhalifu. Askofu Álvarez kwa njia hiyo amekuwa gerezani tangu mwezi Februari mwaka 2023 baada ya kuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Agosti 2022.
Pamoja na Monsinyo Avilés na Padre Treminio, idadi ya mapadre waliokamatwa nchini Nicaragua katika majuma yaliyopita inaongezeka hadi kufikia sita. Mnamo tarehe 20 Desemba iliyopita, Polisi walimkamata pia Askofu mwingine, Isidoro del Carmen Mora Ortega, mwenye dhamana ya Jimbo la Siuna. Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, yeye pia alikamatwa kwa sababu ya kumuombea hadharani Askofu Álvarez wakati wa mahubiri yake. Pamoja na Askofu Mora, waseminari Alester Sáenz na Tony Palacio pia walikamatwa.