Papa Francisko: Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Papa Francisko: Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko: Dumisheni Injili ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo!

Wanawake hawa walikuwa na kila sababu ya kufurahia kutokana na miujiza iliyotendwa ndani mwao, mwaliko ni tafakari ya kina kuhusu uwepo wa Mungu kati ya waja wake na kwamba, huruma na upendo wake unamwandama mwanadamu kwa njia ya zawadi ya maisha, kwa kila mtoto anayebebwa tumboni mwa mama yake, kama ilivyo kwa wanawake wengi na kati yao kuna wale ambao wanatazamia kwa imani na matumaini kuzaliwa kwa watoto wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupokea zawadi ya uhai kwa moyo wa upendo, shukrani na ukarimu. Hata watoto ambao hawajazaliwa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jamii isipojifunza kuwalinda na kuwatunza watu dhaifu, sheria ya mwenye nguvu mpishe, itatawala dunia! Baba Mtakatifu anasema, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Wao ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya wokovu, ni amana na utajiri wa Kanisa. Wao ni dira na ufunguo wa kuingilia mbinguni. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linataka kujitosa kuwahudumia kwa ukarimu na upendo, watoto wadogo ambao bado hawajazaliwa zaidi ya wengine wote, kwani hawa ni watu wasio na ulinzi wala hatia. Inasikitisha kuona kwamba, katika baadhi ya nchi, utamaduni wa kifo unalindwa kisheria, jambo linalokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ikumbukwe kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu yanapaswa kulindwa na kuendelezwa. Utoaji mimba si kitendo cha maendeleo bali ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu! Kanisa lingependa kuwasaidia wanawake kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa kulea na kutunza vyema watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu! Hii itawezekana ikiwa kama haki msingi zitadumishwa na kuendelezwa; wanawake watawezeshwa kiuchumi ili kupambana na umaskini wa hali na kipato! Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, kitendo cha utoaji mimba ni uhalifu na ukatili mkubwa! Madaktari watambue kwamba, wamekula kiapo cha kulinda na kudumisha uhai wa binadamu! Kifo laini ni kielelezo pia cha utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini kwenye Tafakari kutoka katika Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, baada ya kuonesha dalili za kuwa na mafua makali.

Papa ametumia fursa hii kubariki Sanamu za Mtoto Yesu
Papa ametumia fursa hii kubariki Sanamu za Mtoto Yesu

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio, Mwaka C wa Kanisa, Dominika tarehe 22 Desemba 2024 inamweka Bikira Maria mbele ya macho ya waamini. Bikira Maria ambaye baada ya kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, anakwenda kwa haraka kumtembelea binamu yake Elizabeti ambaye katika uzee wake alikuwa ni mjamzito. Rej. Lk 1:39-35. Wanawake hawa wawili waliokuwa wamebeba ndani mwao zawadi kubwa: Bikira Maria alikuwa na mimba ya Mtoto Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu na Elizabeti alikuwa amembeba Yohane Mbatizaji atakayemwandalia Masiha njia. Rej. Lk 1:13-17. Wanawake hawa walikuwa na kila sababu ya kufurahia kutokana na miujiza iliyotendwa ndani mwao, mwaliko kutoka kwa Mwinjili Luka ni tafakari ya kina kuhusu uwepo wa Mungu kati ya waja wake na kwamba, huruma na upendo wake unamwandama mwanadamu kwa njia ya zawadi ya maisha, kwa kila mtoto anayebebwa tumboni mwa mama yake, kama ilivyo kwa wanawake wengi na kati yao kuna wale ambao wanatazamia kwa imani na matumaini kuzaliwa kwa watoto wao. Huu ni mwaliko wa kuonesha mshangao kwa uzuri wa watoto hawa kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Elizabeti. Akina Mama wabarikiwe na kumtukuza Mungu kwa zawadi na muujiza wa uhai.

Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Katika kipindi hiki kuelekea Sherehe za Noeli, sehemu mbalimbali zinapambwa kwa taa na muziki wa Noeli. Lakini, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kuonesha furaha pale wanapokutana na wanawake wajawazito au wale wanaowabeba watoto wao, tayari kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama ilivyokuwa kwa Elizabeti aliyesema “Umebarikiwa kuliko wanawake wote na mzao wa tumbo lako amebarikiwa.” Rej. Lk 1:42; wamwimbie Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama alivyofanya Bikira Maria akisema, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana.” Lk 1:46. Lengo ni kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kubariki mimba za wanawake wote sehemu mbalimbali za dunia, kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu anayemdhaminisha mwanadamu uwezo wa kutoa zawadi ya uhai kwa watoto. Baraka kwa sanamu za Mtoto Yesu iwe ni alama ya shukrani kwa Kristo Yesu aliyefanyika Mwili, akatwaa hali ya binadamu na kuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Iwe ni fursa ya kushukuru na kuwabariki watoto wote wanaozaliwa sehemu mbalimbali za dunia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaifa yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Bikira Maria aliyebarikiwa kuliko wanawake wote awasaidie waamini kuwa na mshangao na shukrani mbele ya Fumbo la maisha kwa watoto wanaozaliwa!

Injili ya Uhai
22 December 2024, 14:05