2024.12.12 Jumuiya  Comunita' del Seminario Maggiore Interdiocesano, di Santiago de Compostela 2024.12.12 Jumuiya Comunita' del Seminario Maggiore Interdiocesano, di Santiago de Compostela  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa kwa Seminari ya Mtume wa Compostela:msiogope kufungua moyo!

Papa Francisko akikutana na maaskofu,walezi na waseminari Kuu za Majimbo ya Mtume wa Santiago Desemba 12,hotuba aliyowakabidhi anabainisha wasisahau kuwa njiani watakutana na watu mbalimbali,wengine wanaweza kuwa wanapitia nyakati ngumu,wanaumia au hawamjui Mungu.Lakini wao wawe mashuhuda wa furaha yote ya Injili,wakiwapa huruma na faraja ya Bwana ili waweze kuponya malenge ya safari.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na Jumuiya ya Seminari Kuu ya Majimbo ya Compostela, Tui-Vigo na Mondoñedo-Ferrol, Alhamisi tarehe 12 Desemba 2024. Katika ujumbe wake aliowakabidhi, Papa  anawakaribisha wote ambao wanajua vizuri utume mkubwa wa Mtume Yakobo nchini Hispania na sasa wao wamefika Roma kwa ajili ya hija, wakifuata nyayo za Mtume Petro na waamini wengine wafuasi wa Yesu. Na kama wasemavyo katika nchi yao; Safari Njema! Kwa njia hiyo katika Ujumbe wake aliowakabidhi wajisomee, Papa anatambua jinsi ambavyo tangu mwezi Septemba wamekuwa wakipitia hali mpya kama seminari ya "majimbo", inayounganisha majimbo ya  “Santiago de Compostela, Tui-Vigo na Mondoñedo-Ferrol.” Amewashukuru kwa upatikanaji wao. Amewahimiza kusonga mbele kwa nguvu na matumaini mapya.

Taswira ya hija

Papa anaamini kuwa taswira ya "hija" inatosha kuonesha ratiba ya mafunzo wanayofanya. “Kama mahujaji, kwanza kabisa, tunasikia wito, ambao unatusukuma kutoka ndani yetu wenyewe; kisha, tunazindua tukio na kuanza kutembea, tukipitia matukio na hatua tofauti. Hatimaye, tunafika mahali pa kulengwa. Vivyo hivyo katika mafunzo ya ukuhani, ambapo lengo ni kuweza kuwa wachungaji wa Watu wa Mungu, wachungaji waliofinyangwa kadiri ya kipimo cha Moyo wa Kristo, wanyenyekevu na wenye huruma. Papa Francisko anabainisha wao kukumbuka kwamba hawako peke yao kwenye safari, hii ni ya msingi: wasiogope kufungua moyo wao kwa Bwana na kuruhusu wasindikizw naye, ili watengeneze maisha yao.

Msisahau kuwa njiani kuna watu wanapitia nyakati ngumu

Pia Papa amesema kwamba wasisahau kuwa njiani watakutana na watu mbalimbali, wengine wanaweza kuwa wanapitia nyakati ngumu, wanaumia au hawamjui Mungu. Lakini wao wawe mashuhuda wa furaha yote ya Injili, wakiwapa huruma na faraja ya Bwana ili waweze kuponya malenge ya safari. Papa pia anawasisitizia waseminari hao kuwa wasiache kuwa mishale ya njano ambayo, kama Mtakatifu Yohane Mbatizaji, alielekeza kwa Yesu na kumwambia kila mtu, kwa maneno yao, lakini pia na zaidi ya yote kwa njia yao ya maisha: kwamba “Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu” (Yh 1, 29). Papa Francisko katika ujumbe wake huo aidha anageukia tukio muhimu linalokaribia kwamba: “Mwaka Mtakatifu wa 2025 unakaribia, kwa neema hii ya Jubilei tuliyopewa tunaendelea kutembea pamoja kama mahujaji wa matumaini, kuelekea nchi ya mbinguni. Yesu awabariki na Bikira Mtakatifu awalinde. Na tafadhali, mkirudi, mwombe mtume Yakobo aniombee.”

Papa na waseminari wa Compostela
12 December 2024, 11:16