Papa Francisko:Upendo wa Kristo unapitia katika ibada na matendo ya dhati
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 4 Desemba 2024 alituma ujumbe kwa washiriki wa Kongamano la Pili la Kimataifa la 'Udugu na Ucha Mungu wa watu' lililofanyika huko Seville nchini Hispania. Alifungua ujumbe wake uliosomwa na Katibu Msaidizi wa Vatican, kama mjumbe wake Maalum, Askofu mkuu Edigar Penna Parra, ambapo kwa kutambua ujitoaji wa kipekee wa watu wa Seville, ambao wanaishi kwa bidii maonesho ya imani yao hadi kuwa sehemu muhimu ya mfumo wao wa kijamii. Imani hii hai, kwa upande wa Baba Mtakatifu alibainisha kuwa si tu safari ya kibinafsi bali ni ya jumuiya inayounda maisha ya Kanisa.
Papa Francisko aliendelea kusisitiza kwamba ufanisi wa kweli wa ucha Mungu unaopendwa na watu wengi upo katika uwezo wake wa kumleta Kristo duniani. Alimnukuu Mtakatifu Manuel González, ambaye alielezea maisha ya Kikristo kama safari ya kwenda na kurudi, ambayo huanza, safari ya nje, katika Kristo na kuishia kwa watu, na huanza ndani ya watu, safari ya kurudi, na kuishia katika Kristo. Safari hiyo, alieleza, inawakilisha kiini cha utume wa Kanisa kuwaleta watu karibu na Mungu. Papa Francisko pia alisisitiza umoja unaopatikana katika utofauti wa ibada hizi. Alieleza jinsi ambavyo mambo mengi ya kipekee, huduma, na kazi nyingi, pamoja na saburi na subira, zinapatana. Kwa sababu iwe kubeba msalaba au kuandamana tu katika maombi, inakuwa ni shauku ileile, upendo uleule na kutengeneza upatano wa pamoja unaofichua uzuri wa Kristo. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko alitoa wito kwa waamini wote kuendelea kumpeleka Kristo mitaani, ili wote wautazame uzuri wake.
Akizungumzia kuhusu machozi yanayomwagika wakati wa ibada, Papa aliyaita machozi hayo kama matendo ya huzuni na upendo ambayo ni mambo ya kumpenda Mungu, na ambayo yanaweza kuonekana kuwa hayaeleweki kwa wengine lakini ni ushuhuda wenye nguvu wa imani. Katika hiyo pia alimnukuu Mtakatifu Manuel kwa mara nyingine tena, aliposema, kwa “watu [...] wana njaa ya ukweli, upendo, ustawi, haki, mbinguni, na labda, bila kutambua, kwa Mungu." Papa kwa hiyo aliwataka waamini kuitikia njaa hii kwa njia ya matendo ya upendo, kuleta huruma ya Mungu kwa wale wanaoteseka katika mwili na roho. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuhitimisha ujumbe wake aliwahimiza washiriki wa Kongamano hilo kuendelea na hija kwa kufuata mfano wa Mchungaji Mwema. Iwapo kubeba msalaba au chini ya vazi la Mama Yake aliyebarikiwa, tunahisi kwamba sisi ni shamba la Mungu, mbegu ya ufalme ibada hizi si desturi tu bali ni njia za kuleta upendo wa Kristo duniani.